![]() |
Martin Odegaar akiwa kwenye moja ya michezo ya Stromsgodset |
Na Ramadhani Ngoda.
"Kila mchezaji ana ndoto za kuchezea Real Madrid," ni maneno yaliyowahi kutamkwa na wachezaji wengi mashuhuri duniani akiwemo nyota wa Ureno na Madrid, Cristiano Ronaldo wakati akikaribishwa Santiago Bernabeu.
Ni vigumu kujiweka mbali na uhalisia huo wakati mwingine. Ni klabu kubwa yenye mafanikio ya kila aina barani Ulaya na duniani kwa ujumla.
Mataji 10 ya ligi ya mabingwa barani Ulaya zamani likiitwa kombe la Ulaya inaweza kuwa moja ya mafanikio hayo.
Lakini katika shauku hiyo ya chungu ya wachezaji kutaka kuingia katika 'bwawa' hilo la mataji na mafanikio, kunaweka mashakani vipaji vya baadhi ya chipukizi ambao wangeweza kuwa zaidi ya nyota nje ya Madrid.
Idadi ya vipaji vilivyopata kustawi Bernabeu na mifano ya makinda waliowahi kutimkia kwingine ni baadhi tu ya viashirio kuwa mahala hapo sio sahihi na rafiki kwa vipaji vinavyochipukia.
Tazama kikosi cha kwanza cha Real, nani mwenye umri chini ya miaka 22? Bila shaka Francisco Roman Alarcon Suarez 'Isco' ndio 'anawaamkia' wote ndani ya kikosi hicho. Wapi nafasi ya Martin Odegaard mwenye miaka 16 tu sasa?
Kwa umri wake ilikuwa ni vigumu kuziba masikio dhidi ya tetesi za kuhitajika na Real Madrid, hata baba yake mzazi mzee Hans Eric alifaharika na taarifa hizo.
"Sishawishiki unaponambia kuwa yeye kwenda Madrid ni uamuzi mzuri.....angekuwa mwanangu nimngemshauri aende Ajax," alisema Michael Laundrap ambaye pia ni nyota wa zamani wa klabu hiyo inayojulikana kwa kulea vipaji nchini Uholanzi.
Inawezekana Lundrap amezungumza hivyo kwa sababu anaijua Ajax kwa uleaji wake vipaji, au haoni Odegaard akipata kung'aa mbele ya kina Greth Bale, James Rodriguez na Toni Kroos.
Kwangu mimi ni bora angewauliza Juan Mata, Javi Garcia, Juanfran na wengine wengi ambao walitimka klabuni hapo kabla ya vipaji vyao havijateketea.
Au hata kiwango cha Borjan Krkic akiwa Stoke City baada ya kuondoka FC Barcelona, ingeweza kuwa darasa kabla ya maamuzi.
Waswahili husema, "mwanga wa tochi hauonekani juani," kwa Madrid ya mastaa na sera ya kusajili majina makubwa kila msimu, Odegaard amenunua kisu cha kipaji chake.
No comments:
Post a Comment