Na
Ramadhani Ngoda
Waswahili
husema, “mazoea hujenga tabia”. Na hii ndio inayoonekana katika soka letu kwa
sasa ambapo ambapo mambo madogo madogo hukomaa na kuwa tabia za vilabu vyetu
hapa nchini jambo ambalo linapeleka soka la nchi hii kusiko.
Ni
wazi sasa kauli ya kiingereza inayosema “they are hired to be fired”
inayotafsirika “wanaajiriwa ili watimuliwe” inaonekana kuthibitika zaidi ktika
soka.
Kutimuliwa kwa kocha wa Yanga Marcio Maximo ambaye pia aliwahi kuwa kocha wa timu ya
taifa ya Tanzania baada ya mchezo dhidi ya watani wao wa jadi Simba, ni sehemu
ya utimilifu wa kauli hii.
Ni
imani yangu kuwa uongozi wa klabu ya Yanga uliangalia uwezo wa kocha huyu
hususani kipindi chake alichoinoa Taifa Stars na kujiridhisha kuwa anaweza kuwa
mbadala sahihi wa kocha Ernie Brandts ambaye naye alikumbwa na “mafuriko” haya.
Nakumbuka
jinsi ambavyo watu walivyofurika katika mitaa ya Twiga na Jangwani wakati wa
kumpokea kocha Ernie Brandts, wengine wakianzia uwanja wa ndege wa J.K Nyerere
kuonesha shauku yao kwa kocha huyu lakini ilimuwia kusahau mapokezi yote
aliyopewa wakati anawasili baada tu ya mabao matatu ya Simba katika mchezo wa
nani mtani jembe msimu uliopita. Brandts alifungashiwa akaenda.
Leo
tunashuhudia Mbrazil Maximo aliyetua kwa mbwembwe katika kazi yake ya pili ya
ualimu Tanzania akiongozana na Wabrazil wenzake Jaja na Coutinho naye
anafungashiwa virago ugonjwa ukiwa ni ule ule ulioua kibarua cha Brandts wa mechi
dhidi ya Simba.
![]() |
Kocha wa Yanga, Hans Van Pluijm |
Sasa
pengo lake limezibwa na kocha aliyewahi kuinoa timu hiyo kabla ya kwenda
Uarabuni kuinoa klabu ya Al Shoula, Hans Van Der Plujim.
Misemo
ya wahenga bado itatawala ikiwemo huu “mwenzako akinyolewa zako tia maji”.
Maneno haya ni vizuri aambiwe kocha Hans kutokana na yeye kurudi kuvaa viatu
alivyoaviacha msimu uliopita na hajui kama vitakuwa saizi yake au vitakuwa
aidha vikubwa ama vidogo kwake.
Na
kama ugonjwa huu wa makocha kupoteza vibarua katika mchezo wa watani wa jadi,
bado kuna mchezo wa Simba na Yanga wa ligi kuu katika mzunguko wa pili, je
hautakuwa ‘ebola’ kwa kibarua chake?
Sote
tunamtakia kila la kheri katika kibarua chake licha kutolewa katika robo
fainali ya michuano ya mapinduzi lakini ana kila sababu ya kuliangalia hili.
Inaonekana kutolewa robo fainali mapinduzi si shida, wala sare na Ruvu si tatizo ila mchawi wa ni mechi ya Simba.
Na
vilabu vyetu viweke wazi kuwa vinaajiri makocha kwa ajili ya michezo gani kwa
sababu, tumeona Maximo ameiongoza Yanga kwenye michezo tisa akishinda mitano(ya
mashindano) na kupoteza mitatu ukiwemo wa nani mtani jembe lakini pointi 15
alizovuna Mbrazili huyu zilionekana nyepesi kwenye mzani wa tathmini kuliko 9
alizopoteza ikiwemo pointi 3 za mchezo usio wa kimashindano(nani mtani jembe).
Sasa
tujiulize, hata Maximo angeipa ubingwa Yanga na kupoteza mchezo dhidi ya Simba
tu, pia angefungashiwa virago?
Ni
kweli David Moyes alitimuliwa kutokana na kupoteza mchezo dhidi ya Manchester
City? Mbona Mourinho hakutimuliwa wakati anatandikwa goli tano pale Camp Nou
akiwa na Real Mdrid? Au mbona hatukuona kutimuliwa kwa Diego Simeone baada ya
kupoteza kwa mabao 4-1 katika mchezo wa fainali wa ligi ya mabingwa dhidi ya
wapinzani wao wa jadi Real Madrid kule Estadio
Da Luiz msimu uliopita?
Au
kuna vipengele vya kimkataba wanavyosaini makocha hawa juu ya mchezo wa Simba
na Yanga? Kunaweza kukawa na maswali mengi juu ya hili lakini bado kuna sababu
ya jitihada za makusudi za kulinusuru soka la nchi yetu kwa kutafuta tiba
ya’ugonjwa huu.
No comments:
Post a Comment